Thursday, December 19, 2013

JINSI YA KUJIFARIJI KIPINDI CHA MATATIZO AU SHIDA ZINAPOKUSONGA....




KWA bahati mbaya watu wengi hawatambui kitu kinachofariji, ndiyo maana wanakimbilia kutegemea msaada. Lakini ukweli ni kwamba mawazo yetu ndiyo faraja pekee ya maisha.

Tukijikubali, kujipenda na kujiwazia mema hatutafadhaishwa na hali ya wenzetu kutojali shida zetu, badala yake tutafurahia matatizo yetu kwa  tarajio la  “yote yanayopita”.

JE, UNAJUA TOFAUTI YA UBINAFSI NA BINAFSI?

Watu wengi hawafahamu tofauti kati ya maneno haya, kutojua huko ni msingi wa matatizo ya kimaisha kwa wanadamu wengi na ukosefu wa faraja.

Kama lilivyo jina la kolamu yangu JITAMBUE,  watu wengi hawajitambui na kujithamini, ndiyo maana wanadhani wamezaliwa ili wateseke hapa duniani.

Ni ukweli usiopingika kwamba kila mmoja wetu angejua kusimama vema kwenye mhimili wa maisha yake tungepunguza kwa kiasi kikubwa mfadhaiko wa mioyo yetu na msongo  wa mawazo usiokuwa na sababu.

Ifahamike kwamba mwanadamu wa kwanza aliumbwa BINAFSI (Mwanzo 2:7,”…mtu akawa nafsi hai) Tafsiri ya neno hilo inayopatikana kwenye kamusi ya Kiswahili Sanifu na TUKI toleo la pili ni “kwa nafsi yangu, kwa  ajili yangu mwenyewe tu.” Mwisho wa kunukuu.

Popote pale duniani mwanadamu binafsi ndiye mwenye  kuishi kwa furaha,  ndiye mwenye mafanikio, anayeweza kujifariji mwenyewe kwa umaskini wake, hali yake duni, ugonjwa wake sugu, taabu na shida zake kwa sababu yeye ni mwenyewe tu.

Katika hali ya  kawaida, nyuma ya binafsi kuna ubinafsi ambao unaelezwa kwenye kamusi “ni hali ya mtu kujifariji na kujipenda yeye mwenyewe” Mwisho wa nukuu ambayo kwa mtazamo inaelea hewani na kuwafanya wengi wadhani kuwa maana ya maneno haya ni moja.
Ingawa mimi si mhubiri lakini ni  mchunguzaji wa maandiko matakatifu ambayo yananirudisha kwenye kitabu cha Mwanzo 3:4-5 ambapo  nabaini mwanzo wa ubinafsi ulivyoanza kwa binadamu wa kwanza.

Nukuu ya maandiko hayo inasomeka hivi: Nyoka akamwambia mwanamke, hakika hamtakufa, kwa maana Mungu anajua ya kwamba  mtakapokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho nanyi mtakuwa kama Mungu kwa kujua mema na mabaya. Hapa wanadamu hawa wa kwanza wanatamani kuishi kwa ubinafsi, wanataka kufanana na Mungu wao.

Ubinafsi halisi ninaouzungumzia ndiyo huu, ambao unamfanya mwanamke ambaye hajazaa atamani kuzaa kama fulani, amiliki gari, awe na maisha ya juu.  Mawazo hayo humsogeza kwenye hali ya kujidharau na hatimaye kufadhaika.

Hii ndiyo sumu ya ubinafsi ambayo inaua, inadhoofisha na  kuondoa hali ya uthubutu wa kukabiliana na matatizo yetu  kama wanadamu na kutufanya tulilie kusaidiwa au kufarijiwa na wenzetu.

Msomaji wangu, kuanzia leo fahamu kwamba ukifadhaishwa na chochote ujue unaumizwa na ubinafsi wako unaokusumbua kutaka uwezo wa mali za mtu mwingine uwe nazo wewe.

Amini usiamini, mtu mwenye mawazo ya ubinafsi ikitokea eneo  lote analoishi watu wote ni  wagonjwa kama yeye, hawajaolewa, hawana kazi,  na maskini, utashangaa kuona mwanadamu huyo anaishi kwa furaha, si kwa  sababu  amefanikiwa, bali amekosa aliyemzidi  wa kujifananisha naye. Usijiumize kwa kutaka maisha ya mtu fulani yawe yako kwa ghafla.
Share this article :

0 comments:

Post a Comment

News Update :
 
Copyright © 2013. Gsmmbaga@gmail.com - All Rights Reserved
Author: charlie | Powered by: .
Designed by: Mmbaga
^